Wewe ni mwanafunzi wa chuo kikuu na darasani mpo wanafunzi 20. Kila mmoja wenu anataka kuanzisha biashara, lakini mnajua pia hamna uwezo wa mtaji wa kuanzisha biashara mmoja mmoja lakini kama mkiunganika, basi siku mkipata boom kila mtu darasani anatoa asilimia 50% ya boom lake na kwa pamoja hela mlizopata mnaziwekeza kwenye biashara mliyoichagua kwa pamoja. Kila mmoja wenu atakua na umiliki wa asilimia 5 wa hiyo biashara.

Kwa lugha nyingine kwenye ushirika huu mshirika mmoja analeta unga mwingine analeta maji na mwingine analeta mboga  tunasonga ugali tunakula. Wote tumechangia katika upatikanaki wa ugali na mwisho wa siku kila mtu anamega tonge kulingana na uwekezaji aliofanya. Kama ulileta unga robo unakula matonge ya robo tu, kama ulileta chumvi unamega tonge moja tu na mwendo unakuwa ni huo wa kulipwa faida kulingana na kiwango ulichowekeza na aliyeleta mboga nyingi au unga mwingi ndio anakuwa na sauti zaidi jinsi ya ugali utakavyopikwa, nani atapika na mpaka namna utakavyoliwa.

Mfano wa Mwisho ni ule wa mtandao wa Twitter ulionunuliwa na Elon Musk, sasa unaitwa X na Elon aliinunua Twitter kwa wastani dola bilioni 44. Ni hela ndogo sana hiyo, pocket money kwa Elon Musk lakini cha kushangaza alizungusha bakuli, kutafuta partners wakuwekeza nae na walijitokeza wengi sana na kwa haraka sana. Hela hiyo tumejairibu kuileta katika pesa za kitanzania na kalkuleta yetu imegoma. Lakini ni kama trilioni 110, ambayo ni zaidi ya pato la taifa la mwaka la nchi nyingi za kiafrika.

Maudhui hapa ni kuwa unapofikiria kuwekeza usifikirie kuwekeza peke yako, unaweza ukasubiri sana. Tafuta mtu, partner, muwekeze naye sababu:-

Mtu mmoja huwezi kuwa wewe ndio unajua kila kitu katika biashara. Kama wewe unajua kuanzisha biashara basi inawezekana usijue namna ya kuiendesha, na wakati huohuo anaejua kuindesha anaweza asijue chochote kuhusu kuuza na masoko, wa masoko anaweza asijue chochote kuhusu mahesabu na kutunza fedha, hivyo basi, mnapokuwa wengi maana yake na ujuzi unakuwa mwingi pia. Mnasaidiana na kugawana majukumu.

Faida ya pili kuwa ukishirikiana na wenzio ina maana na gharama za kuanzisha pamoja na kuendesha biashara pia mnachangia. Biashara nyingi hutumia zaidi ya miaka miwili mpaka zitengamae na kuanza kujiendesha zenyewe. Katika mazingira haya kama muwekezaji ni mmoja tu bila msaada wowote basi anaweza kulazimika kufunga duka na kukubali hasara. Lakini mkiwa wengi na wote mna vyanzo vingine vya mapato basi inakuwa rahisi kuisapoti biashara hata kwa miaka mingi mpaka itakaposimama yenyewe.

Faida ya tatu ipo kwenye mitizamo, mkiwa wengi mnakuwa na mitizamo tofauti na hivyo kuiwezesha biashara kuona vitu ambavyo mtu mmoja peke yake hawezi kuviona. Mfano mtu mmoja anaweza asiione fursa au hatari iliyo mbeleni lakini mkiwa wengi ni rahisi kulichambua au kuliona jambo katika mitizamo tofauti na hivyo kuweza kuepuka hatari au kuchukua fursa zilizo mbeleni.

Kifo cha wengi ni kizuri kuliko kufa mwenyewe. Hamna aliyewahi kufa akarudi na kutuambia hivyo lakini ni mtizamo tulioukuta humu duniani na katika mada yetu tunamaanisha mnapowekeza wengi halafu biashara ikafa yale maumivu au hasara mnamkuwa mmeibeba wengi jambo ambalo ni bora zaidi. Katika tasnia ya sanaa kama vile kuimba au sinema huwa tunasikia wimbo au sinema imeandikwa na fulani, kaimba mwingine, umerekodiwa na mwingine, utasambazwa na kampuni nyingine, masoko wengine, wanasheria wengine na kadhalika.Mara chache sana kusikia msanii kaandika yeye, kaimba, kafanya production, kasambaza na vitu kama hivyo na hivyo basi kama ni wimbo au sanaa yoyote ile isipofanya vizuri sokoni basi watu watakuwa wamegawana hasara.

Sababu ya Nne ni kuwa vichwa vingi ni bora kuliko kichwa kimoja. Mnapokuwa zaidi ya mmoja katika biashara ni rahisi kukabiliana na changamoto zozote zile mtakazokutana nazo. Mtu anakuwa na watu wa kuongea nao na kujadiliana nao changamoto lakini pia hata kwenye mafanikio mnashsreheea wote.

Steve Jobs aliwekeza Steve Wozniack, hivyohivyo kwa akina Larry Page wa Google, alikuwa na mwenzake, Bill gates alikuwa na Mwenzake na ki ujumla ukifiria kuwekeza na kama unafikiria mbali basi utatafuta partner wa kuwekeza nae.

Kama umeamua kupika maandazi basi saka partner muwe wawili au zaidi, kama ni kukodisha movie tafuta wenzio muunganike, kama ni software tafuta mwenzio, kama ni Website au chochote kile, badala ya kulia lia huna mtaji na uwezo mdogo basi unganika na wenzio. Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, ulifundishwa darasa la 2.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *