Wafanyabiashara wengi tumepitia na bado tunaendelea kupitia changamoto za kukosa hela ya kuendeshea biashara. Mtu kila siku unauza lakini hela yako yote inarudi humo humo kwenye biashara na hupati chochote zaidi ya hela ya kula tu. Muda wa kodi ukifika mpaka ukakope mahali ndio uweze kulipa kodi frame, hela ya kununulia malighafi ya kutengenezea bidhaa za kuuza nayo inakuwa shida…..Hapa GIF tumepitia sana changamoto hizo na zifuatazo ni njia kadhaa unazoweza kutumia kupambana na hali hiyo

  1. Kinga ni Bora

Unapoanzisha biashara ukiweza uwe na fedha ya kuendeshea biashara ya kuanzia miezi sita mpaka mwaka, na hata miaka miwili mbele hasa katika vitengo vyenye gharama sana kama vile mishahara , kodi na malighafi. Biashara mpya inaweza kuchukua kati ya miezi 6 mpaka miaka miwili ndio ianze kutengamaa na kuingiza chochote. Na hata kama mwanzoni ikiingiza hela sana basi jua hapo kati kuna kipindi kigumu kinakuja na itapitia mabadiliko fulani, itapooza kabla ya kuji adjast na kupata spidi yake taratibu ndio iendelee. Kwahiyo ukifungua biashara na ikaingiza hela sana mwanzoni usikimbilie kununua iphone mpya, gari au kupaka nyumba rangi, kuna kipindi kigumu kinakuja miezi kadhaa mbele na tumia hiyo hela kuwekeza mahali au weka akiba.

Kama umeanzisha biashara ukiwa na ajira basi usikimbilie kuacha kazi haraka haraka kwani mwanzoni utatumia mshahara wako kuendeshea biashara yako, kama ikifanikiwa. Baki kazini kwanza mpaka ujihakikishie inaweza kujiendesha yenyewe, inaweza kukupa faida wewe na inaweza hata kukopa na kulipa madeni yake yenyewe, au ukianza kuingiza faida (sio mapato, faida tu) inayolingana na mshahara wako uliokuwezesha kuifungua na kuiendesha hiyo biashara.

  • Bei, Mapato na Faida:-

 Hakikisha umeweka bei ya bidhaa yako ambayo imejumuisha gharama zote za uzalishaji na faida yako juu. Ujue tofauti ya mapato na faida. Jitahidi sana usiuze kwa hasara au usiuze chini ya gharama zako za uzalishaji. Kwa hiyo fanya zoezi la kupitia bei ya bidhaa zako na uweke bei inayokulipa. Wakati huohuo, jua tofauti kati ya mapato na faida. Sio hela yote inayoingia ni yako kwani kuna biashara zinatumia malighafi, material, watu na kadhalika na lazima utumie hela ili upate bidhaa ya kuuza. Kwa hiyo lazima ujue hela ya malighafi na uendeshaji ni kiasi gani na faida yako ni kiasi gani ili jioni ukiagiza chips kuku na pepsi ujue unatumia faida na sio faida mpaka na mtaji.

  • Biashara za Ziada

Fikiria mtu una biashara yako unayoitegemea, mathalan  hoteli, ndani ya hoteli unauza vyakula, halafu nje ya hotel una sapoti ya banda la chips, Kuku choma na mishikaki, una fridge mbili za vinywaji, na una sehemu ya juisi, na una kasehemu ka kuuza matunda., ikibidi pop corn na ice cream pia unaweka. Halafu vyote hivi unajaribu kuviendesha kitofauti au peke yake na vinaingiza fedha zake.

 Maana yake nini? Siku biashara yako ya chakula ikienda vibaya huna hata hela ya kununulia mchele na mafuta basi banda la chips nje litakuokoa, utatoa hela huko kwenye chips zije kunyanyua hotelini ndani ili wateja wakija wakute chakula, lakini wakati huo huo pia una sehemu ya juisi, matunda na kadhalika vyote vinakupa sapoti….kwa hiyo hakikisha hutegemei biashara moja tu.

GIF tuna bekari tunauza keki, lakini pia tunauza vifaa vya keki, na tunauza lambalamba na  kadhalika. Siku mtaji wa kwenye keki ukipwaya tunatoa hela kwenye duka la vifaa na biashara inasonga. Isiwe shida. 

  • Kukopa Material

Hakikisha unakuwa na ma supplier wanaokuamini na jenga nao uhusiano nao mzuri tu kiasi kwamba mambo yakiwa magumu dukani kwako basi unaenda kuchukua bidhaa kwa mkopo kwa supplier yako. Cha msingi uhakikishe unamlipa ndani ya siku mbili tatu , usikae sana ili na yeye biashara yake isikwame kwa sababu inawezekana na yeye kachukua mzigo kwa mkopo na mnaishi kwa kutegemeana. Mafanikio yake ndio mafanikio yako.

  • Akiba Kwanza

Kila mara unapopata fedha uwe na ka utaratibu ka kujilipa mwenyewe kwanza. Kwa kujilipa mwenyewe hatumaanishi kuwa ukiuza kitu basi uchukue hela uagize chips kuku na pepsi ya kushushia. Hapana. Kwa kujilipa mwenyewe tunamaanisha ukishauza , chukua kati ya asilimia 20 mpaka 30 na iweke kwenye akaunti ya akiba. Sio uende benki bali weka kwenye akaunti ya akiba kwa simu, au kama una lipa namba ya voda au tigo pesa zote zina option za kupeleka fedha kwa mmiliki. Asilimia 70 inayobaki inarudi kwenye biashara na ikipungua tafuta maeneo mengine ya kukopa au kupunguza gharama na kadhalika lakini usiende kuichukua ile asilimia 30. Hiyo utaitumia hali ikiwa mbaya sana na huna njia mbadala kabisa. Weka akiba kwanza halafu pambana na hali yako.     

  • Bana Matumizi, Funga Mikanda

Wakati mwingine biashara inahitaji kiongozi mzuri tu. Na kiongozi mzuri atajua namna ya kusimamia mapato yanayoingia vizuri. Atapunguza gharama ambazo sio za lazima kila mahali na ataweka mkazo mkubwa kwenye ubunifu wa namna uzalishwaji unavyofanywa ili kupunguza gharama zisizokuwa za lazima.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *